Kijiji cha Namelock eneo la Maungu kaunti ya Taita Taveta ni kijiji ambacho jamii ya Wamaasai ambao ni wafugaji wanaishi. Na kama desturi yao wametegemea sana ufugaji wa ng’ombe katika kukidhi mahitaji ya maisha yao.
Lakini jamii hiyo kwasasa inakumbwa na changamoto chungu nzima za ufugaji. Hii ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanashuhudiwa ulimwengu mzima.
Miriam Kasumuni ni mzee wa nyumba kumi katika kijiji hicho.Ni mama wa watoto 8 na ni mjane. Anasema anahisi mume wake aliaga dunia baada ya kupatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu mwilini.Hii ni baada ya wao kupoteza zaidi ya ng’ombe 100 kwa wakati mmoja.
Sinyati Kiringoli ni mama wa watoto 7. Awali alikuwa na ng’ombe zaidi ya kumi lakini kwa sababu ya ukame, alipoteza ng’ombe hao na kwa sasa anamiliki ngo’mbe 4 pekee.
‘Kiangazi kikubwa kilikuja na mifugo mingi ikaaga dunia, na watu wakabaki na ng’ombe na mbuzi moja ama mbili, mimi nikiwa mmoja wao’,Alisema Sinyati.
Jamii ya wamaasai hasa wanaume kazi yao kubwa ni kuchunga mifugo. Lakini kutokana na wao kupoteza mifugo yao kwasababu ya ukame, kwa sasa wamekosa kazi ya kufanya. Kiasi cha kwamba wameruhusu wake zao kufanya kazi ili kupata angalau pesa kidogo kuangalia familia zao.
Kutokana na hali hiyo, kina mama hao waligeukia ukataji miti ili wauze kuni wapate pesa za kukimu familia zao. Tabia ambayo iliharibu mazingira kwa kiasi kikubwa.Tonkei Kotina alikiri kuwa ukataji wa miti ambao walikuwa wakiendeleza umechangia pakubwa katika mabadiliko ya tabia nchi wanayoshuhudia.
‘Tumekumbwa na janga la njaa kwasababu ya ukame, hii ni kutokana na ukataji wa miti kwasababu ya makaa na ujenzi. Kitambo ilikuwa inanyesha vizuri lakini siku hizi,mvua imepungua sana’, Alisema Tonkei.
Kulingana na mkurugenzi wa shirika linalohusika na utunzaji wa mazingira la African Wildlife Foundation eneo la Tsavo kaunti ya Taita Tavet -Maurice Nyaligo, asilimia 98 ya miti asili kaunti hiyo ya Taita Taveta imeisha.
Hii ni kutokana na ukataji wa miti kwa utumizi wa makaa, ujenzi na kuni.
Tafiti zinaonyesha kuwa wanawake wana uwezekano mkubwa kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi zaidi ya wanaume. Kwani majukumu yao kama walezi huwafanya kuwa katika mazingira hatari zaidi wakati wa mafuriko na ukame unapotokea.
Ili kusitisha uharibifu huo wa mazingira kwa kisingizio cha kuwapatia kina mama hao kipato cha kila kulisha jamii zao, Shirika la Hadithi Crafts lililoko eneo hilo la Maungu lilikuja na mradi wa kushona na kuuza shanga. Ambapo kina mama hao hupewa vifaa vyote hitajika na shirika hilo.
Baada ya kushona shanga hizo, shirika hilo la Hadithi Crafts linazinunua shanga hizo kutoka kwa kina mama hao. Kate Sau ni afisaa msimamizi wa shirika la Hadithi Crafts, alisema mradi huo ni njia moja wapo ya kuwafanya wanawake hao kukoma kukata miti na kuharibu mazingira.Hatua ambayo alisema anaona imeanza kuzaa matunda katika utunzaji wa mazingira.
Mbali na mradi huo kuwa unawasaidia kutunza mazingira, pia unawapatia wanawake hao kipato ambacho kinawasaidia wao kufadhili majukumu yote ya familia.
Kwani, mabadiliko hayo ya tabia nchi yamewaathiri kiasi cha kuwa wamebadilisha majukumu ya familia, ambapo kwa sasa wanawake wanashughulikia majukumu yote ya familia.
Miriam Kasumuni ni miongoni mwa wanawake ambao wamefanya kazi hiyo ya kushona na kuuza shanga kwa takriban miaka 5 sasa. Alisema mradi huo wa kushona ushanga umebadilisha maisha yao si haba.
‘Hii kazi ya kushona ushanga imekuwa Baraka kwetu, kwani najua nikishona sitakosa shilingi hamsini kumpa mtoto wangu kununua kalamu na kununua sare za shule, maisha yamebadilika,sisi wanawake sasa ndio kichwa tunafuga wanaume’, Alisema Miriam.
Tonkei Kotina alijiunga na kikundi hicho baada ya kupoteza ng’ombe zake 20, hivyo asiwe na namna nyengine ya kupata mapato. Lakini alisema kazi hiyo ya utengenezaji wa shanga umemsaidia hata kusomesha wajukuu zake.
Sinyati Kiringoli ni msaidizi wa mwenyekiti katika kikundi chao cha wanawake cha Nasirian eneo la Miasenyi kilicho na wanawake 21.Kulingana na Sinyati, kwa sasa waume zao wanawaruhusu kufanya kazi ili wapate pesa za kulisha familia zao.
Jacob Kasumuni ni miongoni mwa wazee wanaotoka katika kijiji hicho cha Namelock. Kasumuni ana wake wawili na watoto sita. Alikiri kuwa ukame umeathiri pakubwa shughuli zao za ufugaji.
Hatua ambayo alisema ilisababisha wao kubadilisha tamaduni zao na kuruhusu wake zao kufanya kazi ili wapate pesa za kukidhi mahitaji ya familia.
‘Kwasababu mifugo imeisha sasa hakuna vyenye watakaa bure, lazima wajishughulishe ndio tuapte chakula. Utengenezaji wa shanga umetusaidia pakubwa sana kwasababu wakishatengeneza na kuuza kunapatikana chakula na hata dawa za mifugo kidogo iliyobaki’, Alisema Jacob Kasumuni.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa asilimia 80 ya watu wanaolazimika kuhama makazi yao kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ni wanawake.
Hamisa Zaja ni mshirikishi mkuu wa maswala ya mazingira katika baraza la kimataifa la maswala ya mazingira la Green World. Alisema shughuli mbalimbali za kijamii zimeathirika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Hali ambayo imeathiri sana wanawake.
Alitoa wito kwa serikali kuunga mkono juhudi za mashirika mbalimbali yanayowasaidia wanawake hasa walioathirika na mabadiliko ya tabia nchi.
‘Ni vyema kama serikali itawekeza na kuwasaidia wanawake kwa maswala ya maji ambayo yatawasaidia kwa ukulima na pia maji yatawasaidia hata kupika chai kama watakosa kabisa chakula, hivyo hawatalala njaa’, Alisema Hamisa.